RSS Feed

Tag Archives: usafi

Uchafu katika Miji: Jukumu la Nani?

Posted on

Nimekuwa nikiangalia kwa makini sana namna ambavyo miji yetu na hasa majiji ambavyo yamejawa na uchafu kila kona.

Kinachosikitisha zaidi ni kuona jinsi hata maeneo kama vile mabonde ya mito yalivyogeuzwa kuwa madampo. Hali inatisha kiasi cha kusikitisha.

Ukiwauliza wenyewe (Halmashauri za miji, manispaa na majiji; unapewa jibu moja: “usafi wa miji ni jukumu la kila mtu”. Nasema hivi: hiyo si kweli. Sidhani kwamba serikali kuu haitengi kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya usafi wa miji yetu. Na kama hilo fungu hutengwa, linatumikaje? Mbona miji kama Moshi imeweza kutunza usafi wake? Na kwa nini manispaa, miji na majiji yetu yasifanye ubunifu na kutafuta vyanzo vya mapato kwa kufanya usafi wa mitaa?

Siamini kwamba tumeshindwa kabisa kuifanya miji yetu kuwa safi.

Kipindupindu Hatukiwezi

Posted on

Ugonjwa wa kipindupindu huwa unasababishwa na kitu kimoja tu — kula kinyesi cha binadamu. Unaweza kula kinyesi cha binadamu kupitia njia mbalimbali: 1) Kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi 2) Kushiriki chakula wakati ulitoka chooni na hukunawa mikono 3) Kunywa vinywaji vilivyoandaliwa bila kuzingatia kanuni za usafi n.k.

Dawa ya kipindupindu ni moja tu — usafi. Na hapa ni usafi katika ujumla wake — wa binafsi na ule wa jamii. Na hapo ndipo ugumu wa kupambana na kipindupindu unapokuja. Kwa sababu wewe binafsi unaweza kujitahidi na kuwa msafi; ila kama jamii inayokuzunguka si safi bado huwezi kuuepuka. Usafi wa jamii kwa nchi zetu hizi za ulimwengu wa nne ni kama hauwezekani.

Ili ufanye usafi kwa nia ya kuondoa ugonjwa wa kipindupindu unahitaji mifumo, miundombinu na vitendea kazi ambavyo kwa viongozi tulio nao utaimba tu miaka hadi miaka ila sidhani kama kuna ambaye atakusikiliza. Gharama zake ni kubwa mno.

Usafi (ule wa jamii na hata wa binafsi) unahitaji maji — maji mengi sana. Kwa familia ya kawaida tu; ili kuwa na usafi wa kawaida tu, yanahitajika madumu kama nane ya maji kwa siku. Si familia nyingi zinaweza kumudu gharama kama hii.

Ukweli ni kwamba hata huku mjini tunakopita kila siku vinyesi vimetapakaa kila mahali. Unapopita mitaa ya posta na kukuta mimaji fulani michafu michafu inatiririka barabarani au miferejini ujue katika mimaji hiyo kuna kinyesi pia. Na hatuwezi kujua inawezekana hii mimaji inaweza kuwa inaingia kwenye vyakula vingi tunavyonunua na kula.

Watu wengi wanaoishi mijini ni kwamba bado wanatumia vyoo vya shimo. Mvua zinaponyesha hivi vyoo vinatiririsha mavi (kinyesi) na uchafu huu aghalabu huingia katika vyanzo vyetu vya maji tunayotumia majumbani.

Utaona sasa jinsi vita ya kupambana na kipindupindu katika mazingira kama haya ilivyo ngumu. Tunaiweza? Jibu ni hapana, hatuiwezi.

Tufanyeje?
Jitahidi uwezavyo kwa level yako wewe kama mtu binafsi – nawa mikono baada ya kutumia choo. Hakikisha chakula unachotumia kimeandaliwa katika mazingira masafi. Kama ukiweza, kunywa maji uliyochemsha wewe mwenyewe.

KILIMO KWANZA!

Follow

Get every new post delivered to your Inbox.