“Tunamwitaji atakayeoteshwa kuhusu ‘dawa’ ya kumaliza matakataka mijini. Na mwingine aoteshwe ‘dawa’ ya kuwaondoa wapiga debe mijini. Mwingine aoteshwe ‘dawa’ ya kuwaondoa wafanyabiashara wanaopanga bidhaa mabarazani na njiani.”
Hivyo ndivyo ilikuwa ikisema “status update” yangu kwenye facebook. Nilisukumwa kuandika huo ujumbe kwa sababu ya mambo ambayo yamekuwa yakitokea katika nchi yetu kwa siku za karibuni.
Tumekuwa tukisikia kila kukicha juu ya watu ambao wanadai kuwa “wameoteshwa” na mungu (lower case m) dawa ya magonjwa sugu yanayowakabili waTZ. Mambo yalianzia Loliondo au ‘kwa Babu’ kama wengi wetu tunavyopenda kupaita. Ilianza kwa mchungaji mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwaisapile, “kuoteshwa” dawa ya magonjwa sugu.
Baada ya hapo umefuata utitiri wa watu ambao kila kukicha wamekuwa wakiibuka na kudai kwamba “wameoteshwa” juu ya dawa ambayo ‘hakuna ugonjwa ambao haitibu’ — ukiamini. Ukiamini nini? Ni swali ambalo watu, hata waliotumia hiyo dawa, hawawezi kukwambia. Ukimwamini Mungu? Ukiliamini neno la Mungu? Ukiiamini dawa? Ukiamini kwamba dawa ile inaponya? Ukimwamini mtoa dawa? Ukiuamini mrigariga? UKIAMINI NINI?
Nilishasema hapo awali na ninarudia kusema: jamii ya Watanzania inayo ‘magonjwa’ sugu mengi ukiachilia ya kisukari, UKIMWI, kansa, stroke, shinikizo la damu, presha, vidonda vya tumbo n.k. Tunayo ‘magonjwa’ ambayo yanahitaji ‘tiba’ isiyo ya kawaida. Je nani atathubutu kujitokeza akadai kuwa “ameoteshwa” kuyatibu haya magonjwa?
Ni nani ataoteshwa ‘dawa’ ya foleni mijini? Nani ataoteshwa ‘dawa’ ya ukosefu wa maji vijijini? Nani ataoteshwa ‘dawa’ ya kukatikakatika kwa umeme? Nani ataoteshwa ‘dawa’ ya uchafu unaozagaa kila kona katika miji na majiji yetu? Nani ataoteshwa ‘dawa’ ya kupanda bei kwa bidhaa kila kukicha? Nani ataoteshwa ‘dawa’ ya umaskini? Nani ataoteshwa ‘dawa’ ya mikataba mibovu? Nani? Nani?
Ila sasa, Je, akijitokeza atakayeoteshwa ‘dawa’ ya magonjwa haya TUTAMSHABIKIA? Je, tutapanga foleni kumpa sapoti? Je, tutajipanga nyuma yake na kumwambia, “tuna imani na wewe”? Je, tutaamini?
Rafiki yangu mmoja akaniambia na hapa namnukuu: “Magufuli alioteshwa dawa ya kuondoa kero za barabara mbovu. Je, uliona kilichompata?” Sote tunajua kilichompata. Hatukumwamini. Hatukuamini!




