RSS Feed

Tag Archives: maendeleo

Kama ningekuwa Kiongozi wa “Chama”/Serikali

Posted on

Hivi karibuni nchi yetu imeshuhudia sarakasi za kisiasa zinazozihusisha pande mbili. Upande mmoja ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) au serikali na kwa upande mwingine ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kwa yule (yeyote) ambaye amekuwa mfuatiliaji wa siasa za Tanzania tangu ulipoingia mfumo wa siasa za vyama vingi hapa nchini atakubaliana na mimi kwamba kwa sasa mazingira ya kisiasa ya nchi yetu yamebadilika sana. Mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 tulishuhudia chaguzi ambazo zilivihusisha vyama vingi. Ukilinganisha na chaguzi zote za nyuma, ule wa 2010 umekuwa ni uchaguzi ulioibua mambo mengi.

Kuna watu ambao hawakuridhishwa kabisa na namna ambavyo Tume ya Uchaguzi ya Tanzania ilisimamia uchaguzi huo. Kuna ambao wanasema hadi leo kwamba asilimia ya wananchi iliyojitokeza na hatimaye kumchagua Rais ilikuwa ndogo kiasi ambacho kinatia doa (mashaka) ushindi wake. Na kwa mara ya kwanza nchini Tanzania tuliona Rais aliye madarakani akishinda kwa asilimia isiyozidi 70. Yote hayo ni ya kweli. Lakini pia tumeona kitu kingine cha tofauti – hali ya siasa baada ya uchaguzi!

Katika miaka mingine yote tulizoea kuona vyama vya upinzani “vikipotea” mara tu baada ya uchaguzi. Hali hii ilikifanya chama kinachokuwa madarakani na serikali yake vikifanya kazi kwa “ku-relax” – kwa raha zake. Vyama vya upinzani vilikuwa vikitoweka katika ulingo wa siasa na kuibuka tena miaka minne baadae. Hii iliwafanya hata wale waliokuwa madarakani kufikia hatua ya kuviita vyama vingine eti “vya msimu” – seasonal political parties. Hali hii imebadilika kabisa na sasa walio madarakani hawajui wafanye nini kuikabili.

CHADEMA mara tu baada ya uchaguzi hawakulala. Walijipanga kimkakati kwenda nchi nzima wakiwaelimisha wananchi juu ya matatizo yao na umuhimu wa kuwawajibisha viongozi wao. CHADEMA wanapita huko na huko wakiwaambia wananchi mapungufu na madhaifu ya serikali yao. Lengo la CHADEMA, na kwa hakika lengo la chama chochote cha upinzani duniani, ni kutafuta udhaifu wa chama na serikali inayotawala na kutumia udhaifu huo kuingia madarakani. CHADEMA wakikakaa na kusubiri uchaguzi mwingine hawataweza kuifikisha elimu ya kisiasa kwa wananchi, wananchi hawatafunguka macho na utawala utaendelea kuwa wa CCM. Hilo halina ubishi na hilo ndiyo hofu kuu waliyonayo CCM na serikali yake.

Wanachotakiwa kufanya CCM/Serikali:

Ili kukabiliana na wimbi hili la mapinduzi/mabadiliko linalotembea nchi nzima kwa sasa, serikali haitakiwi kufanya makosa wanayofanya sasa hivi. Kosa la kwanza ambalo serikali inafanya ni KUFANYA SIASA (kama CHADEMA) kuliko KUFANYA MAENDELEO. Huu ni mwanzo wa kupoteza vibaya. Badala ya kuingia kwenye ulingo wa siasa, serikali inatakiwa ijikite kwenye shughuli za maendeleo zenye kuonekana. Fanya juhudi nzito ya KUZALISHA UMEME WA KUTOSHA na uusambaze huo umeme kwa wananchi kwa bei nafuu. Zibane mamlaka za maji na uhakikishe wananchi wanakuwa na VYANZO VYA UHAKIKA VYA MAJI SAFI NA SALAMA – mjini na vijijini. Kaza program ya UJENZI WA MABARABARA (RELI) nchi nzima kwa kasi ya kutisha. Weka vizuri vitengo vya mipango-miji kwa kuanzisha MAKAZI BORA na kupunguza FOLENI katika barabara za mijini. Fukuza kutoka kwenye chama na ndani ya serikali WATENDAJI WAZEMBE NA WALA-RUSHWA. Acha Kiswahili cha “tuache tu mahakama na vyombo vyetu vya sheria viwashughulikie.” – lini? Kwa mkakati wa namna hii CHADEMA haitawanyima usingizi. Hamtatumia mabilioni ya shilingi kujinadi wakati wa kampeini. Hiyo ndiyo akili.

Nani Anaongoza?

Posted on

Wako wapi akina Warioba wa leo?

Wako wapi akina Sokoine wa kizazi hiki?

Nani atupatie Augustine Mrema sasa?

Ah! Nimeanza waraka wa Jicho  kwa maswali mengi leo. Ila ukiwa Mtanzania na una uchungu na nchi yako ukiyaona yanayofanyika na usiwe na maswali tunaweza kuutilia shaka uzalendo wako. Kuna kipindi imefikia hatua nika-conclude kwamba hii nchi yetu (Tanzania) inajiendesha yenyewe tu. Tukitumia mizani ya moja hadi kumi (a one-to-ten scale) na tukasema 1 inawakilisha hali duni na kumi inasimama kwenye kilele cha ubora; ninaweza kusema kwamba hapa tulipofikia (Tanzania) tuna namba 2 au 3 – kiutendaji. Mambo hayafanyiki. Watendaji hatuwajui, hawaonekani.

Enzi zile akina Warioba walisema, walitoa amri, mambo yakafanyika. Akina Sokoine hawakuwahi kufanya urafiki na ulaghai, ughoghoi wala uvivu. Walikuwa wasemaji, wafuatiliaji na wachapakazi. Ulikuwa ukifanya kazi chini yao halafu ukazembea wasingekuonea haya hata kidogo. Walikuwa tayari kufa kwa ajili ya maendeleo ya watu wao. Hawakuogopa.

Japo umaarufu wake kisiasa ulikuja kushuka kwa sababu ambazo wanaozijua si wengi ila tulio wengi tutamkumbuka mtu aliyejulikana kwa jina la Augustine Lyatonga Mrema. Enzi zake watu walifanya kazi bwana. Huyu bwana alipewa wizara moja tu lakini kwa sababu ya utendaji wake hata watendaji wa wizara zingine walikuwa wanatekeleza wajibu wao ipasavyo. Hakuwa lelemama tena. Hakucheka na mtu ilipokuja kwenye masuala nyeti ya maendeleo ya wananchi.

Leo hii tumebaki na usemi mmoja – Tanzania ni nchi ya amani. Hii si kweli hata kidogo. Nani kakwambia hii ni nchi ya amani? Amani na ujinga wapi na wapi? Amani ipi wakati siwezi kuendesha gari yangu na kusimama kwenye mataa bila kufunga (tight) vioo vya gari yangu? Mtu unaibiwa kila kitu mchana-mchana tena kwenye mataa ukisubiri taa ya kijani iwake. Amani ipi wakati asilimia 90 ya wananchi wote (milioni 40) wanaishi kwa kipato cha chini ya dola moja kwa siku? Amani ipi wakati Tanzania inaongoza kwa idadi ya vifo vya akina mama na watoto walio chini ya miaka mitano tena kwa magonjwa yanayotibika? Ni amani gani unayosema wakati kila wiki tunapoteza maisha ya watu wapatao 20 kwa ajali za barabarani? Amani au ujinga?

Huku Temeke ninapoishi ukitembea njiani unajisikia vibaya. Takataka zimejaa kila kona hadi katikati ya barabara. Watu wanajimwagia uchafu popote wanapotaka, wakati wowote. Hakuna anayeweza kuwazuia. Nani? Marundo ya takataka za kila namna zimetapakaa na wala hakuna anayejali. Halafu jinsi tulivyo wajinga unaweza kukuta mamilioni ya pesa yanatengwa kila mwezi kwa ajili ya usafi wa Temeke na inaishia mifukoni mwa wajanja wachache. Haiingii akilini kusema kwamba halmashauri kama ya Temeke haina ofisi inayohusika na usafi. Na unaweza kukuta jamaa aliyewekwa kwenye kitengo cha usafi anatembelea Toyota Land Cruiser ya milioni 150. Unachojiuliza ni hiki: anapita wapi? Jibu lake ni rahisi: anapita juu ya takataka. Takataka haziwezi kumsumbua yeye hata kidogo kwa sababu gari “yake” ina AC (kiyoyozi) na muda wote anakuwa amefunga vioo – shauri yenu.

Tunasikitisha. Tunatia kinyaa. Tunasubiri UN, World Bank na IMF waje kufagia barabara zetu. Thubutu. Kwao hata vumbi hakuna. Kula kwetu vumbi kwao ni mradi. Fungu za fedha zitatengwa tutakapougua kutokana na hili hili vumbi na wao watapewa hizo fedha na kuja huku kutalii.

Follow

Get every new post delivered to your Inbox.