RSS Feed

Tag Archives: daladala

Mapinduzi ya daladala

Posted on

Leo wakati nakuja katikati ya jiji la Dar es salaam nilipata bahati ya kupanda ‘daladala’ nzuri yenye heshima na utulivu. Huwa ninatokea kituo ama cha Davis Corner (Tandika) au Mwembeyanga. Nyakati za asubuhi katika vituo nilivyovitaja hapo juu hali ya usafiri kwa kweli huwa ni mbaya sana. Si rahisi kupanda gari kwa ustaarabu bila kusukumana na hata wakati mwingine kuibiwa vitu vyako.

Nilipofika Mwembeyanga leo nikamkuta kijana kama kawaida akipiga debe, “Posta, posta moja kwa moja mia tano. Posta mia tano moja kwa moja hiyoooooo.” Ilikuwa ni gari aina ya Toyota Coaster nzuri imesafishwa na viti vizuri vya kukalia. Kwa kweli ilikuwa inavutia. Sikuona kwa nini nisilipe mia tano na kutumia usafiri wenye ustaarabu kuliko kung’ang’ania kulipa 250 na kukipata cha mtema kuni.

Nilichokuja kugundua baadae ni kwamba huyu bwana alituleta mjini leo si yeye peke yake anayefanya hivyo. Wako wengi. Ila cha kusikitisha ni kwamba wanafanya kazi hii kwa kujificha. Swali ninalojiuliza ni hili: Kwa nini wasitangaziwe kwamba kama kuna mtu ana gari lake zuri nyakati za asubuhi wakati kuna shida ya usafiri ni ruhusa kupeleka watu mjini kwa gharama yoyote ambayo abiria wanaosubiri watakuwa tayari kulipa? Ningekuwa mhusika wa mambo ya usafiri katika jiji la Dar es salaam ningetoa tangazo la hivi:

“KAMA UNA GARI YAKO NZURI NA UNGEPENDA KUPAKIA ABIRIA WAKATI KUNA SHIDA YA USAFIRI (HASA ASUBUHI NA JIONI) UNARUHUSIWA KUTANGAZA KIASI CHOCHOTE CHA NAULI AMBACHO ABIRIA WATAKUWA RADHI KULIPA ILI UWAPELEKE WAENDAKO”.

Kwa namna hii tutasababisha ushindani wa wenye magari kuwakimbilia abiria wakiwaomba wapande magari yao na hii adha ya abiria kugombea magari itaisha. Pia hata wenye magari yao binafsi ambao huwa wakitoka kazini anaingia yeye mwenyewe na kuendesha gari la watu sita akiwa peke yake wanaweza kuwa wakitafuta walau mchango wa mafuta kwa kupakia abiria wawili au watatu nyakati za asubuhi au jioni.

KILIMO KWANZA!

Mvua imeanza Dar

Posted on
Jiji la Dar es salaam leo limepata baraka za mvua

Jiji la Dar es salaam leo limepata baraka za mvua

Usafiri wa umma (mijini) Tanzania

City public transport in Tanzania is not suitable for children, the elderly and diabled

City public transport in Tanzania is not suitable for children, the elderly and disabled

Leo wakati nakuja kazini nilitumia usafiri wa daladala. Pale nilikopandia daladala kulikuwa na akina mama ambao umri wao ulikuwa umeenda kidogo. Kwa kweli niliwahurumia. Hakuna jinsi ambavyo unaweza kupanda daladala bila kusukumana. Na kwa umri wa hao mama zangu nilikuwa na wasiwasi kwamba kwa kweli ingewawia ngumu kupata usafiri.

Ukijaribu kuangalia usafiri wetu wa umma hasa ule wa mijini utakubaliana na mimi kwamba si usafiri ambao watoto, wazee na wenye ulemavu wanaweza kuutumia bila matatizo.

Si wazee wengi wanaoweza kupanda gari kwa kupitia dirishani. Si watoto wengi wanaweza kusukumana ili kupenya kwenye mlango na kuingia ndani ya basi. Wala si walemavu wengi wanaoweza kubanana kwenye gari ili waweze kufika waendako.

Hili ni tatizo la kiuongozi kwani kuwa na usafiri wa kistarabu mijini inawezekana. Inaweza kufanyika kirahisi zaidi kuliko KILIMO KWANZA.

Follow

Get every new post delivered to your Inbox.