RSS Feed

Tag Archives: amani

Kukata tamaa: Je, ni hulka ya Watanzania?

Posted on

“Sitaenda kwenye maandamano. Hata tukiandamana hakuna kitakachobadilika.” Iliuwa kauli ya kwanza ya Mtanzania mmoja. Mwingine naye, “Nendeni tu kwenye mkutano. Mtakalolizungumza lolote kwangu ni sawa tu. Hata hivyo hiyo mikutano haina maana yoyote.” Sasa iliyonishangaza na kunikera zaidi ilikuwa hii:

“Hii ni Tanzania bwana. Mtapiga kelele weeee ila hakuna kitakachofanyika. Kujihusisha kwenye mambo ya siasa ni kazi bure. Wewe fanya mambo yako. Tafuta chakula cha familia yako. Jitafutie maendeleo yako mwenyewe. Achana na mambo ya kitaifa. Acha kabisa kuongelea siasa za nchi.”

Hizi ni kauli za watu waliokata tamaa. Ni kauli za Watanzania wengi: vijana na hata wazee. Ni watu waliochoka. Mbele yao wanaona bahari na nyuma yao majeshi ya Farao. Wamefika mwisho. Hawana tumaini. Ila kauli hizi si za kupuuza hata kidogo. Hizi ni kauli-sumu kwa taifa ambalo linataka kupiga hatua ya kimaendeleo.

Ni kauli zenye nia ya kuzima dhamira za watu ambao wangependa kudai haki zao. Ni kauli ambazo viongozi wazembe, wavivu na wabadhirifu wangependa kuzisikia. Kibaya zaidi: hizi ni kauli ambazo zaweza kuleta kizazi cha watu waoga, wasiopenda kuhoji nchi yao inaendeshwaje. Ni mawazo-mgando. Mawazo hatari!

Mtanzania yeyote anayetoa kauli za hivyo usidhani kuna siku atamkemea mtoto wake asijihusishe na wizi wa mali za umma. Na wala sidhani kama watoto wa mtu mwenye mawazo kama haya wanaweza kufikiri kwamba wizi wa mali za umma ni jambo baya. Tutaleta Tanzania kizazi kisicho na maadili kwa sababu kizazi chetu kimekuwa ni chenye kupuuzia.

Shime Watanzania, tuamke! Zi wapi nyimbo zetu za kizalendo? Zi wapi kauli zetu za ukombozi? U wapi ujasiri wetu wa kale? Ni nini kimetupata?

Nani Anaongoza?

Posted on

Wako wapi akina Warioba wa leo?

Wako wapi akina Sokoine wa kizazi hiki?

Nani atupatie Augustine Mrema sasa?

Ah! Nimeanza waraka wa Jicho  kwa maswali mengi leo. Ila ukiwa Mtanzania na una uchungu na nchi yako ukiyaona yanayofanyika na usiwe na maswali tunaweza kuutilia shaka uzalendo wako. Kuna kipindi imefikia hatua nika-conclude kwamba hii nchi yetu (Tanzania) inajiendesha yenyewe tu. Tukitumia mizani ya moja hadi kumi (a one-to-ten scale) na tukasema 1 inawakilisha hali duni na kumi inasimama kwenye kilele cha ubora; ninaweza kusema kwamba hapa tulipofikia (Tanzania) tuna namba 2 au 3 – kiutendaji. Mambo hayafanyiki. Watendaji hatuwajui, hawaonekani.

Enzi zile akina Warioba walisema, walitoa amri, mambo yakafanyika. Akina Sokoine hawakuwahi kufanya urafiki na ulaghai, ughoghoi wala uvivu. Walikuwa wasemaji, wafuatiliaji na wachapakazi. Ulikuwa ukifanya kazi chini yao halafu ukazembea wasingekuonea haya hata kidogo. Walikuwa tayari kufa kwa ajili ya maendeleo ya watu wao. Hawakuogopa.

Japo umaarufu wake kisiasa ulikuja kushuka kwa sababu ambazo wanaozijua si wengi ila tulio wengi tutamkumbuka mtu aliyejulikana kwa jina la Augustine Lyatonga Mrema. Enzi zake watu walifanya kazi bwana. Huyu bwana alipewa wizara moja tu lakini kwa sababu ya utendaji wake hata watendaji wa wizara zingine walikuwa wanatekeleza wajibu wao ipasavyo. Hakuwa lelemama tena. Hakucheka na mtu ilipokuja kwenye masuala nyeti ya maendeleo ya wananchi.

Leo hii tumebaki na usemi mmoja – Tanzania ni nchi ya amani. Hii si kweli hata kidogo. Nani kakwambia hii ni nchi ya amani? Amani na ujinga wapi na wapi? Amani ipi wakati siwezi kuendesha gari yangu na kusimama kwenye mataa bila kufunga (tight) vioo vya gari yangu? Mtu unaibiwa kila kitu mchana-mchana tena kwenye mataa ukisubiri taa ya kijani iwake. Amani ipi wakati asilimia 90 ya wananchi wote (milioni 40) wanaishi kwa kipato cha chini ya dola moja kwa siku? Amani ipi wakati Tanzania inaongoza kwa idadi ya vifo vya akina mama na watoto walio chini ya miaka mitano tena kwa magonjwa yanayotibika? Ni amani gani unayosema wakati kila wiki tunapoteza maisha ya watu wapatao 20 kwa ajali za barabarani? Amani au ujinga?

Huku Temeke ninapoishi ukitembea njiani unajisikia vibaya. Takataka zimejaa kila kona hadi katikati ya barabara. Watu wanajimwagia uchafu popote wanapotaka, wakati wowote. Hakuna anayeweza kuwazuia. Nani? Marundo ya takataka za kila namna zimetapakaa na wala hakuna anayejali. Halafu jinsi tulivyo wajinga unaweza kukuta mamilioni ya pesa yanatengwa kila mwezi kwa ajili ya usafi wa Temeke na inaishia mifukoni mwa wajanja wachache. Haiingii akilini kusema kwamba halmashauri kama ya Temeke haina ofisi inayohusika na usafi. Na unaweza kukuta jamaa aliyewekwa kwenye kitengo cha usafi anatembelea Toyota Land Cruiser ya milioni 150. Unachojiuliza ni hiki: anapita wapi? Jibu lake ni rahisi: anapita juu ya takataka. Takataka haziwezi kumsumbua yeye hata kidogo kwa sababu gari “yake” ina AC (kiyoyozi) na muda wote anakuwa amefunga vioo – shauri yenu.

Tunasikitisha. Tunatia kinyaa. Tunasubiri UN, World Bank na IMF waje kufagia barabara zetu. Thubutu. Kwao hata vumbi hakuna. Kula kwetu vumbi kwao ni mradi. Fungu za fedha zitatengwa tutakapougua kutokana na hili hili vumbi na wao watapewa hizo fedha na kuja huku kutalii.

Follow

Get every new post delivered to your Inbox.