Ya Yanga, CECAFA, TANESCO na Tanzania
Jana ilikuwa fainali ya Kombe la CECAFA/Kagame. Mechi ilifanyika uwanja wa Taifa, Dar es salaam na Yanga kuibuka mabingwa. Hii ni baada ya wiki takriban mbili za soka lenye siasa nyingi zaidi kuliko ufundi. Kuna ambao walidiriki hata kusema kwamba CECAFA (waandaaji wa michuano) walikuwa na lao jambo katika michuano — kuzipendela timu wenyeji!
Zile timu zilizotoka Kenya, Uganda, Eritrea, Somalia, Rwanda na Burundi zilikuwa zikilalamika kwamba timu za Tanzania zinapendelewa. Nasikia kuna siku timu ya Yanga walirudia penati mara mbili. Mtu mmoja akasema ati: refa ni kama vile alikuwa anahakikisha Yanga hawakosi penati. Madai haya inawezekana ni ya kweli. Lazima tukubali kwamba ili kuendesha mashindano kama haya CECAFA wanahitaji pesa — ya kwao kwanza — viongozi wa CECAFA na kidogo kinachobaki kinaenda kuendeleza soka! Hongera. Nikolas Musonye anaweza kuwa na mawazo tofauti.
Hayo tuwaachie kina Musonye na president wake, Tenga. Kilichonichefua zaidi hiyo jana ni pale ambapo umeme ulikatika uwanja wa Taifa na uwanja mzima ukawa giza. Aibu ya mwaka! Wakati wachezaji wakielekea kupewa zawadi na kukabidhiwa kombe, TANESCO wakawaonyesha CECAFA na ulimwengu kwamba wao ndiyo mabingwa. Jitihada za mheshimiwa waziri, Dr. Nchimbi, kuwasiliana na TANESCO ili umeme urudi hazikufua dafu. Ikabidi watu
wawashe simu zao za tochi au tochi zao za simu — asante Mchina — umetujengea uwanja, umetuletea na simu za tochi.
Tanzania kama nchi tulitia aibu ya mwaka kwani ikumbukwe kwamba fainali hizi za Kagame zilikuwa zikirushwa moja kwa moja na kituo maarufu cha mambo ya soka duniani — SuperSport. Kile kilichotokea pale uwanjani hata mtangazaji wa SuperSport alishikwa na kigugumizi kukielezea.
Long live Yanga, long live CECAFA, TANESCO and Tanzania. Wiki njema!
Advertisement

